Pageshttps://www.insidehighered.com/views/2020/02/05/why-institutions-should-continue-support-their

Graduation

Graduation
From left: Jumanne Hussein, Dr.Suru, Mzee Gantala, Dr. Masoud during the graduation ceremony held on 26th November, 2015 at Chimwaga Hall, Dodoma

Tuesday, August 27, 2013

Ya Rugambwa Yametimia

Kona ya Karugendo
Ya Rugambwa yametimia, ya Mwoleka je?
Privatus Karugendo
Toleo la 263
17 Oct 2012
TULIPOMZIKA marehemu Laurian Kadinali Rugambwa, kwa mara ya kwanza mwaka 1997, Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Mhashamu Askofu Nestory Timanywa, aliwatangazia waumini, waombolezaji na viongozi wa vyama vya siasa na serikali kwamba mwili wa Laurian Kadinali Rugambwa, ungetunzwa kwa muda kwenye kanisa la Kashozi na baada ya miaka miwili, ungehamishiwa kwenye kanisa kuu la Bukoba. Wakati huo Kanisa Kuu la Bukoba, lilikuwa linafanyiwa ukarabati mkubwa.
Ninakumbuka pia kwamba Policarp Kadinali Pengo, kwenye mazishi hayo hayo ya muda, aliwaambia watu wa Bukoba, kwamba siku ya mazishi rasmi ikifika, wasipomjulisha ili aje kumzika Rugambwa, atawashitaki! Wakati huo alikuwa hajatangazwa kuwa Kadinali, lakini aliongea kwa kujiamini kwamba yeye ndiye mrithi wa Kadinali Rugambwa.
Inashagaza kwamba sasa taarifa zinatujulisha kwamba Kadinali Pengo, hakuweza kumzika Laurian Kadinali Rugambwa, mara ya pili. Lakini ni kitu alichokifahamu na kukibariki.
Na kwa vile wakati wa mazishi ya muda kulikuwa na utata wa kwa nini Laurian Kadinali Rugambwa azikwe Bukoba na si Dar es Salaam, maana yeye alikuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, ukifuata sheria za Kanisa Katoliki na mapokeo, angezikwa Dar es Salaam. Na maneno yakapita kwamba Kadinali Pengo, alikuwa amekataa kumzika Kadinali Rugambwa Dar es Salaam.
Hivyo ilibidi Kadinali Pengo, kufafanua zaidi juu ya Kadinali Rugambwa kuzikwa Bukoba:
Alisema Kadinali Pengo: “… kuna watu wanataka wamfahamu Kadinali Rugambwa, zaidi ya alivyojifahamu yeye mwenyewe. Yeye alijua kwamba kuzikwa Dar es Salaam hakuihitaji kuomba ruhusa, lakini kuzikwa Bukoba, alihitaji kuomba ruhusa. Akachagua la pili la kuomba ruhusa… akachagua kuzikwa huku maporini…Alijua ni mtu muhimu kwenye Kanisa na watu wangependa kutembelea kaburi lake… ingekuwa rahisi kama angezikwa Dar es Salaam, lakini yeye alichagua huku. Tuheshimu uamuzi wake. Uvumi kwamba nimekataa kumzika Dar es Salaam si kweli, kama niliweza kuishi naye akiwa hai, ningeshindwa kuishi naye akiwa kaburini?”
Oktoba 6, 2012 tumeshuhudia masalia ya mwili wa Laurian Kadinali Rugambwa, yakihamishwa kutoka Kanisa la Kashozi na kuzikwa rasmi katika kanisa kuu la Bukoba. Ni baada ya miaka 15 ya mazishi ya muda, na si baada ya miaka miwili kama alivyoahidi Askofu Nestory Timanywa wakati ule mwaka 1997.
Sitaki kungia kwenye mjadala wa ni kwa nini mazishi haya yalichelewesha hivyo au ni kwa nini ukarabati wa kanisa kuu la Bukoba umechukua miaka yote hiyo zaidi ya 17. La muhimu ni kwamba hatimaye yametimia; Laurian Kadinali Rugambwa, amezikwa rasmi kwenye kanisa kuu la Bukoba.
Maandalizi ya mazishi haya, ushiriki wa watu na mapenzi ambayo watu walionyesha kwa kitendo hiki cha kuhamisha masala ya mwili wa Kadinali Rugambwa, kutoka Kashozi na kwenda kuyazika Bukoba ni ishara ya kutosha kwamba hata waumini hao walikuwa wanasubiri kwa hamu tukio hilo.
Hata kama wangeambiwa kulibeba jeneza hilo kwa mikono na kutembea kwa miguu kutoka Kashozi, zaidi ya kilomita 25, hadi Bukoba mjini, wangefanya hivyo. Walisubiri miaka 15, kuona wosia wa Kadinali Rugambwa wa kuzikwa rasmi unatimizwa.
Makala hii imelenga kuwashukuru Mwadhama Policarp Kadinali Pengo na Mhashamu Askofu Nestory Timanywa, kuheshimu wosia wa marehemu Laurian Kadinali Rugambwa. Ingawa sijapata kujua kama huo wosia wa Kadinali Rugambwa ulikuwa wa kuandikwa au wa mdomo, kwa vile Mwadhama Kadinali Pengo, alitamka mwenyewe juu ya wosia huu na Askofu Timanywa akasisitiza juu ya wosia huu ni lazima tuamini.
Katika hali ya kawaida na tena bila lawama yoyote ile na kwa kulindwa na Sheria za Kanisa, Kadinali Pengo, angeziba masikio na kumzika Kadinali Rugambwa Dar es Salaam. Hakuna mtu angepinga uamuzi huo. Lakini kwa hekima na busara, Kadinali Pengo, aliamua kuheshimu wosia wa Kadinali Rugambwa, wa kuomba kuzikwa Bukoba.
Hivyo mwaka 1997, alipoaga dunia, mwili wake ulisafirishwa na kusindikizwa hadi Bukoba. Mtihani ukabaki kutimiza ombi la kuzikwa kwenye kanisa kuu la Bukoba, maana wakati ule lilikuwa linafanyiwa ukarabati. Ndipo uamuzi ukafikiwa wa kuuzika mwili wa Kadinali Rugambwa kwa muda kule Kashozi.
Kila mtu ana mapungufu yake. Mwadhama Laurian Kadinali Rugambwa, alikuwa mtu wa kimataifa. Kwa nafasi yake ndani ya kanisa angeweza kuzikwa hata Roma, maana kila Kadinali ana kanisa lake kule Roma.
Alihamishwa Dar es Salaam kutoka Bukoba. Wakati akiwa Dar es Salaam alifanya kazi kwa moyo wote bila kufikiria nyumbani kwao Bukoba. Hivyo angeweza hata kuzikwa Dar es Salaam. Lakini kumbe ndani kabisa ya moyo wake, bado alitamani azikwe nyumbani kwao. Hayo ndiyo yalikuwa baadhi ya mapungufu yake yeye kama mwandamu.
Baada ya kumzika kwa muda Kadinali Rugambwa kwenye kanisa la Kashozi, Mhashamu Askofu Nestory Timanywa angeweza kupuuza wosia wa kuzikwa kwenye kanisa kuu la Bukoba. Angeweza kusema, ombi la kuzikwa Bukoba, limetimizwa na inatosha. Yeye kama Askofu asingehojiwa na mtu yeyote yule. Sheria za Kanisa zingemlinda.
Lakini kwa heshima na busara aliamua kuheshimu wosia wa Kadinali Rugambwa wa kuzikwa kwenye kanisa kuu la Bukoba. Ndiyo maana hata baada ya miaka 15, kanisa lilipokamilika, Mhashamu Askofu Nestory Timanywa, aliendelea kutekeleza wosia wa kumzika Kadinali Rugambwa kwenye kanisa kuu la Bukoba. Ndiyo maana nimesema kwamba Mhashamu Askofu Nestory Timanywa, anastahili pongezi kubwa kwa kuheshimu wosia wa marehemu.
Wakati yamefanyika mazishi rasmi ya Kadinali Rugambwa, mwezi huu wa Oktoba, Oktoba 16, tuna kumbuka pia ya miaka 10 ya kifo cha Askofu Christopher Mwoleka, aliyekuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge. Askofu huyu naye aliacha wosia wa kuzikwa kwenye parokia alipokuwa ameanzisha Jumuiya yake ya Mkamilishano.
Aliweka nguvu zake nyingi kujenga Jumuiya hii na alitamani Jumuiya hii iendelee na kustawi na kusambaa jimbo zima la Rulenge. Kwa vile moyo wake wote ulikuwa kwenye jumuiya hiyo, alitamani azikwe hapo hapo. Bahati mbaya wosia wake huo ulitupwa pembeni na wakubwa kuamua kumzika Rulenge, badala ya Parokia ya Bushangaro-Karagwe.
Wakati Kadinali Rugambwa, aliomba kuzikwa Bukoba, na huku aliishi na kufanya kazi Dar es Salaam, Askofu Mwoleka, aliomba kuzikwa ndani ya jimbo lile lile alilokuwa akiliongoza, lakini kwenye parokia na si makao makuu ya jimbo.
Hoja ninayojaribu kuijenga kwenye makala hii ni kwamba kama wosia wa Kadinali Rugambwa wa kuzikwa Bukoba uliheshimiwa, na kama ombi lake la kuzikwa kwenye kanisa kuu la Bukoba limezingatiwa, basi wosia wa Askofu Christopher Mwoleka, wa kuzikwa parokia ya Bushangaro Karagwe, uzingatiwe. Kama masalia ya Mwadhama Rugambwa, yalivyosafirishwa kutoka Kashozi hadi Bukoba mjini na kuzikwa rasmi kwa heshima zote, basi na masalia ya Askofu Mwoleka, wakati tunakumbuka miaka 10 ya kifo chake, yasafirishwe kutoka Rulenge hadi Bushangaro.
Askofu Mwoleka aliacha wosia wa kuandikwa na wa mdomo juu ya ombi lake la kuzikwa kwenye Parokia ya Bushangaro. Bahati mbaya aliyeachiwa wosia wa maandishi naye sasa hivi ni marehemu. Hivyo inaweza kuwa shida kuupata wosia huu wa maandishi. Lakini wale walioachiwa wosia wa mdomo bado wengi wao wako hai na wanakumbuka hata sehemu ya kanisa la Bushangaro, ambako Askofu Mwoleka, alipendekeza kuzikwa.
Mwaka 2002, kilipotangazwa kifo cha Askofu Mwoleka, baadhi ya waumini wa parokia ya Bushangaro waliofahamu wosia wa marehemu, waliaanza mpango wa kuchimba kaburi. Kwa mshangao, wakapata taarifa ya mazishi kufanyika Rulenge.
Hivyo Marehemu Askofu Mwoleka, alizikwa Rulenge, kinyume na wosia wake. Hekima na busara zilizowaongoza Kadinali Pengo na Askofu Timanywa, kuheshimu na kutekeleza wosia wa marehemu Kadinali Rugambwa, hazikujitokeza kusimamia na kutekeleza wosia wa marehemu Askofu Mwoleka.
Waloufahamu wosia wa Askofu Mwoleka, wa kuzikwa Bushagaro, walijitahidi kufikisha ujumbe wa wosia wake sehemu inayohusika. Lakini hawakusilizwa. Hoja ikiwa ni kwamba kinachofuatwa ni Sheria za Kanisa na wala si matakwa ya mtu binafsi!
Tunaambiwa kanisa ni moja, Katoliki la Mitume. Iweje Sheria za Kanisa zifuatwe Rulenge na zisifuatwe Jimbo Kuu la Dar es Salaam? Iweje Sheria za Kanisa zifuatwe Rulenge na zisifuatwe Jimbo Katoliki la Bukoba? Kama mwili wa marehemu Kadinali Rugambwa, ulisafirishwa kutoka Dar es Salaam hadi Bukoba, na kama mwili huo umezikwa mara ya pili kwa kusafirishwa tena kutoka Kashozi hadi Bukoba mjini, kwa nini mwili wa marehemu Askofu Mwoleka usisafirishwe kutoka Rulenge hadi Bushangaro na kuzikwa rasmi kufuatana na matakwa yake?
Uongo ni kitu kibaya, na ninafikiri hakuna mtu anayefurahia kusema na kueneza uongo. Lakini pia mtu akiwa na wasiwasi kwamba alichoambiwa ni uongo, anafanya utafiti, anauliza huku na kule hadi anapata ukweli. Kanisa Katoliki ni taasisi kubwa, ina uwezo wa kufanya utafiti na kuchunguza. Kama wosia wa Askofu Mwoleka, kuzikwa Bushangaro ni uongo unaotengenezwa; uchunguzi ufanyike ili ukweli ubainike.
Ndugu, jamaa, marafiki na waumini wa nje na ndani ya Tanzania, wanatamani kushuhudia marehemu Askofu Christopher Mwoleka, akilazwa kwenye nyumba yake ya milele katika parokia ya Bushangaro-Karagwe.
Kwa miaka 10 nimekuwa nikiandika juu ya maisha ya Askofu Christopher Mwoleka. Ni imani yangu kwamba wasomaji wanafahmu huyu alikuwa ni mtu wa namna gani. Lakini kwa wale wanaotaka kufahamu zaidi juu yake, wanaweza kusoma vitabu vyake, maana yeye aliandika: Do This, The Church as A Family na Katekesi Hai. Lakini pia anatwajwa kwenye vitabu mbalimbali vya Jumuiya Ndogo ndogo, hivyo hata kwenye mtandao habari zake zinapatikana.
Leo hii Jimbo Katoliki la Rulenge, halipo tena. Jimbo hili lilimegwa na kutengeneza majimbo mawili.Jimbo la Kayanga na Jimbo la Rulenge Ngara. Parokia ya Bushangaro, ambako Askofu Mwoleka, alipenda azikwe, iko Jimbo la Kayanga. Na jimbo hili la Kayanga, kwa kutambua mchango wa Askofu Mwoleka, wakati wa uhai wake, wameamua tarehe 16 ya kila mwezi wa 10, iitwe Mwoleka Day.
Hivyo siku hiyo ikifika waumini wanakwenda kwenye Parokia ya Bushangaro, kusherehekea Mwoleka Day. Hivyo mwaka huu ni vyema waumini hawa kusali kwa nguvu, kuomba na kudai mwili wa marehemu Askofu Christopher Mwoleka, uhamishwe kutoka Rulenge na kuzikwa rasmi kwenye kanisa la Bushangaro – Karagwe.

Soma zaidi kuhusu:

No comments:

Followers

UNGANA NA ULIMWENGU WA SELFIE

Habari Bayana

News Alerts