RAI YA
JENERALI
Kuku
tuliowafungulia asubuhi ndio hawa wanarudi
Toleo la 314
4 Sep
2013
INAWEZEKANA kwamba sasa watu wengi zaidi wanatambua
yale yaliyokuwa yakisemwa huku yakibezwa, na wanaona yale waliyokuwa wakiambiwa
waone huku wakikataa kuona, japo wanayo macho.
Tumekuwa na tabia, kwa muda mrefu hadi sasa ni
utamaduni, kwamba tunaposikia jambo lisilotupendeza tunaziba masikio na
tunapoonyeshwa kitu kisichotufurahisha tunafumba macho. Tunasahau kwamba kuziba
masikio au kufumba macho hakulifanyi jambo hilo na wala hakusababishi kitu
hicho kutoweka.
Baadhi yetu tumekuwa tukionya kwamba mambo
tunayoyafanya leo yanazo athari zake kesho na keshokutwa, na kwamba kila tendo
lina tendo-rejea (For every action there is a reaction), lakini bado
tunao watu miongoni mwetu wanaoelekea kuamini kwamba wanaweza kutenda watakavyo
na zisitokee athari zozote.
Mifano ni mingi, lakini inatosha kuchukua miwili au
mitatu. Hivi sasa Tanzania imejijengea sifa ya hovyo, sifa ya aibu, ya kuwa
njia ya mpito (transit) ya dawa za kulevya ziendazo huko ziendako.
Inaumiza roho kila mara unapopata habari kwamba Mtanzania mwingine amekamatwa
akivuka mpaka wa nchi nyingine akiwa amebeba mihadarati.
Kama lilivyosema gazeti moja nchini, Watanzania
wamegeuka ‘punda’ wa kubeba mizigo ya mihadarati ya watu wengine (siku hizi
wabebaji hao wanaitwa makontena kwa sababu ya kubeba dawa hizo tumboni). Maana
yake ni kwamba mizigo wanayobeba si ya kwao, bali wao ni wapagazi wa kuwabebea
hao wenye mizigo yao.
Kwa kuangalia tatizo hili juu-juu, bila uchambuzi
kidogo tunawaona vijana hawa waliogeuka kuwa punda kama wana wapotevu waliokosa
maadili na waliowaasi wazazi wao na wanaolisaliti taifa lao.
Aidha, tumekuwa na janga la baadhi yetu kuwaua na
kuwakata viungo wenzetu wenye ulemavu wa ngozi (albino) kiasi kwamba
dunia nzima sifa moja ya nchi yetu ni kwamba albino hawana usalama hapa. Watu
wengi wanaotupenda wamesumbuliwa na jambo hili, wakijiuliza ni jinsi gani nchi
iliyowahi kuwa na sifa ya utu, uungwana na ukarimu inaweza kugeuka na kuwa na
jamii ya nyang’au kama hawa.
Najaribu kuzichukua sifa hizi mbili za aibu kwa
pamoja, huku nikijaribu kudadisi chimbuko lake na jinsi zilivyojitokeza kuwa ni
sifa za taifa letu. Sifa hizi mbili ni matokeo ya kile nilichokiita
tendo-rejea, ‘reaction.’ Jamii inayoachana na maadili ya uongofu,
ikashindwa kuwafundisha watoto wake jinsi ya kuishi katika uadilifu; jamii
inayoonyesha dhahiri kwamba utajiri kwa njia yoyote ile ni jambo jema na kwamba
ukiiba si tatizo bali tatizo ni kukamatwa; jamii inayotukuza wezi na matapeli,
badala ya kuwasweka jela inawachagua na kuwatuma bungeni, jamii hiyo inalea
punda wa mizigo ya mihadarati.
Hali kadhalika, tunapopuuza elimu yakinifu ya watu wetu
na watoto wetu wakafundishwa kushinda mitihani bila kupata maarifa;
tunapokubali kwamba ‘multiple choice’ ndio wa kupima uwezo wa
mwanafunzi, na tunapowaachia watu wachache wafanye wanachotaka na elimu ya
watoto wetu bila kuwasaili, tunakuza u-mbumbumbu ambao baadaye unajitokeza
katika medani zote za maisha ya jamii yetu, kutoka ngazi za chini hadi za juu.
U-mbumbumbu huu ndio huo unaotufanya tukubali
kwamba kuna mzee mmoja Loliondo anayetibu maradhi halaiki kwa kikombe kimoja na
taifa zima likaonekana liko mbugani kwenda ‘kunywa kikombe.’ Watu wanakufa kwa
kuacha dawa zao, hospitali zinaachia wagonjwa waende kupata ‘kikombe,’ sote
tunaonekana wajinga, lakini mwisho wa siku hakuna mtu wa kutoa maelezo ya
kuridhisha kuhusu hicho ‘kikombe’ na tunajifanya hamnazo, kama vile hakuna
kilichotokea. Tunajibaraguza, hatuoni haya!
Ujuha huu ni ujuha unaoambukiza, haubakii kwa mtu
mmoja mmoja, kwa sababu unayo misingi yake katika elimu ya ujuha, na hii maana
yake ni kwamba mbegu zake zimesambazwa shamba zima.
Sasa, ujuha unaotokana na elimu ya uzuzu
inapokutana na mmomonyoko wa maadili unaotokana na kufundishana wizi, tunakuwa
tumefanikisha kupata muungano baina ya punda wa kubeba mihadarati na dalali wa
kuchinja albino. Hawa wawili, baba yao ni ujinga na mama yao ni mmomonyoko wa
maadili. Mkunga aliyewazalisha ni uongozi mbovu.
Nataka nieleweke kwamba nasema uongozi mbovu ni
wetu sote: Tunajiongoza vibaya, tunaongozana vibaya na tunawaongoza vibaya hao
tunaotakiwa kuwaongoza. Binafsi hupenda kusema kwamba kiongozi si yule
aliyakabidhiwa ofisi kwani huyo ni ofisa tu; kiongozi ni yule anayeonyesha
njia. Katika mambo haya ninayoyajadili sote ni viongozi, na sote tumewasaliti
watu wetu.
Maofisa waliokabidhiwa ofisi hizi tumewachagua
wenyewe, na kwa sababu ofisi hizo wanazozishikilia ni sisi tuliowakabidhi, kwa
kawaida ni juu yetu kuwaandama ili waziendeshe vyema kwa maslahi yetu. Kwa
kweli, ni sisi tunaotakiwa kubeba lawama iwapo tumewakabidhi ofisi zetu watu
wasio na uwezo wa kutufanyia kazi.
Iwapo sisi ni wakweli katika nafsi zetu, iwapo
tutajichunguza kwa undani na kujisaili kwa dhati, tutagundua kwamba masuala
mazito na yenye umuhimu mkubwa tunayachukulia kipuuzi, tunayachezea na
kuyatomasatomasa na kuyatania, kama vile hatujui hatari zinazotokana na upuuzi
huo. Halafu yanapotulipukia, ni kama tunashangaa.
Tunaposhangaa tunataharuki na kuchukua hatua za
kuchekesha – kama tunaweza kucheka -- ambazo hazina chembe ya kuonyesha kwamba
tumetambua chanzo cha tatizo. Hatua tunazochukua ni za kujishikiza tu, kama
vile tunasubiri kitu fulani kitokee ndipo tuokoke, na kwa jinsi hii tunasogea
kwa mtindo wa siku hadi siku, mpaka hapo itakapotokea gharika.
Nakumbushia tena, kila tendo lina tendo-rejea, na
Waingereza wana msemo kuhusu “chickens coming home to roost,” ambao
maana yake ni kwamba kuku unaowafungulia asubuhi usiwashangae ukiwaona wanarudi
nyumbani jioni; ni wako hao, na wanakuja kulala.
Naangalia kila upande, kila idara, kila medani,
kila eneo la maisha (siasa, uchumi, elimu, afya, kilimo, michezo, utamaduni,
maadili) na ninaona kuku wengi wanarudi, mmoja baada ya mwingine, na
nikiwaangalia vizuri na kuchunguza rangi za manyoya yao, naona ni wale wale
kuku wetu tuliowafungulia asubuhi. Sasa tunashangaa nini?
- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/kuku-tuliowafungulia-asubuhi-ndio-hawa-wanarudi#sthash.zWrKtDnV.dpuf
(Chanzo: Raia Mwema).
No comments:
Post a Comment