Nasaha za Mihangwa
Kwa nini
Mlima Kilimanjaro uko Tanzania na si Kenya?
Toleo la 314
4 Sep
2013
MPAKA wa Tanzania na Kenya ni wa ajabu na ni wa
kushangaza pia. Tofauti na mipaka mingine ya nchi yetu upande wa Mashariki,
Kusini na Magharibi, Mpaka huo wa Kaskazini umechorwa kwa mstari ulionyooka
kana kwamba ulichorwa kwa msaada wa rula kuanzia Bahari ya Hindi, kuelekea
Kaskazini hadi Ziwa Victoria.
Kwa jinsi ulivyoanza, mstari huo ulipaswa kwenda
moja kwa moja Kaskazini Magharibi, na kuutupa nje Kaskazini Mlima Kilimanjaro
uwe ndani ya Kenya, badala ya kuwa Tanzania ilivyo sasa. Lakini, pengine kwa
sababu maalumu, mchoraji aliupaisha juu Kaskazini zaidi makusudi ulipokaribia
Mlima huo, kisha ukapinda tena kuelekea Kaskazini Magharibi kwa unyoofu ule
ule, kuhakikisha kwamba Mlima wote unakuwa ndani ya Tanzania badala ya Kenya;
na kuendelea hadi Ziwa Victoria kwa kunyooka vivyo hivyo.
Kwa nini, nani kitu gani hasa kilimfanya mchoraji
wa Mpaka huo kupindisha mstari huo kufanya Mlima Kilimanjaro uwe nchini
Tanzania, badala ya kuwa nchini Kenya?
Mnyukano wa Wajerumani na Waingereza
Kuna dhana inayovuma kwamba, Malkia wa Uingereza,
Victoria; alimpa zawadi mjukuu wake, mtawala (Emperor) wa Ujerumani, Wilhelm
Mlima huo mwaka 1886, kwa sababu mjukuu huyo alipenda vitu vikubwa. Dhana
hii si sahihi kwa sababu mwaka huo, Wilhelm hakuwa mtawala wa Ujerumani, bali
Babu yake. Lakini jibu sahihi linatokana na Mataifa ya Ulaya kugombea Afrika
(Scramble for Africa), mnyukano uliokamilishwa na Mkutano wa Berlin kwa mataifa
hayo kukaa meza moja kuchora mipaka (partition) kuigawana Afrika.
Mnyukano huo ulishika kasi ya kutisha katikati ya
miaka ya 1880, Uingereza ikiongoza na kufuatiwa na Ufaransa; huku Ujerumani
nayo ikijikakamua kutoachwa nyuma katika kuwania makoloni.
Desemba 4, 1884, Sultani Mangungu wa Usagara
(Msovelo) alisainishwa Mkataba wa “Urafiki” na Jasusi la Kijerumani, Karl
Peters, bila kujua kwamba alikuwa anauza nchi yake kwa Wajerumani na kuitwa
“Deutch –Ostafrika”, yaani “Afrika Mashariki ya Wadachi/Wajerumani” na
kuimilikisha Kampuni ya Kijerumani iliyojulikana kama “German East African
Company” (GEAC).
Februari 1885, Karl Peters aliomba ulinzi wa
Kampuni yake kwa Kiongozi wa Ujerumani (Emperor), Bismarck, na kupewa barua ya
kukubaliwa (Imperial Letter of Protection) kupata ulinzi wa maeneo (nchi) yote
yaliyochukuliwa na GEAC upande wa Bara Magharibi mwa Dar es Salaam, na maeneo
ya Uzigua, Ukaguru na Usambara ambako machifu 10 wa maeneo hayo walisaini
Mikataba “kumuuzia” nchi zao bila kujua.
Ilichotaka GEAC ni kupata njia huru na Bandari
kwenye Bahari ya Hindi, na hivyo kuzua mgongano na Sultani wa Zanzibar
aliyeshikilia Pwani yote, kutoka Somalia upande wa Kaskazini hadi Rasi Delgado
(Msumbiji) upande wa Kusini; na pia Bara yote iliyokuwa njia ya misafara ya
Watumwa hadi Maziwa Makuu.
Na pale Sultani Sayyid Barghash alipoonesha jeuri
ya kutokubali matakwa ya Wajerumani, Manowari ya kivita ya Kijerumani ilitia
nanga Bandari ya Zanzibar na kuelekeza mitutu ya mizinga kwenye Kasri lake,
naye akasalimu amri hima. Wakati huo Zanzibar ilikuwa chini ya usimamizi
na ulinzi wa Uingereza (British Protectorate) kwa Mkataba maalumu.
Kuona hivyo, Februari 26, 1886, Waziri Mkuu wa
Uingereza wa wakati huo, Lord Salisbury, aliingilia kati akiamini kwamba, haki
za Zanzibar juu ya eneo lote la Pwani zilikuwa wazi, ingawa hakuwa na uhakika
juu ya ukomo wake Kaskazini (Somalia?), lakini alifikiri umbali wa maili 60
ulimtosha Sultani. Alijua kuwa, himaya ya Sultani ilijumuisha pia Wilaya za Kilimanjaro
na Uchagani; alisema: “Eneo lote la Wilaya ya Kilimanjaro kamwe haliwezi
kuwa chini ya ulinzi wa bendera nyingine (mbali ya Sultani au Uingereza) bila
kuathiri maslahi ya Uingereza”.
Wababe wote walikuwa na mikataba
Ni kwamba, Waingereza, Wajerumani na Sultani
mwenyewe, wote walikuwa na mikataba waliyoingia na Machifu wa Kichaga kutambua
himaya za wababe hao, kama tu alivyofanya Chifu Mangungu. Mmoja wa
Mikataba ya Machifu hao 25 na Sultani, uliotiwa sahihi Mei 30, 1885, ulisomeka
hivi:
“Sisi Masultani (machifu) wa Uchagani na
Kilimanjaro, tunaapa mbele ya Jenerali Mathews na Askari wake na Wafuasi,
kwamba, tunatambua kuwa (sisi) ni watawaliwa wa Mtukufu Sultani wa Zanzibar, na
hivyo tunapeperusha bendera yake juu ya minara nchini mwetu kuthibitisha utii
wetu kwake, na kuwa,tunamtambua kama mtawala/mfalme wetu”.
Mkataba huo wa pamoja ulitiwa sahihi (dolegumba) na
Machifu Mandara wa Moshi, Kitungeti wa Kirua; Marealle wa Muranju (Marangu),
Mitanuvi wa Mamba, Fumba wa Kilema, pamoja na Machifu wa Machame, Rombo, Taveta
na wengineo.
Mandara alitia sahihi Mkataba mwingine kama huo na
Mjerumani wa GEAC, Dakta Karl Juhlke, Juni 11, 1885, kumpa mamlaka yote na haki
ya kuchukua na kutumia ardhi, kutoza kodi na ushuru, pamoja na kuanzisha
utawala wake na Mahakama; kuvuna Mlima Kilimanjaro, Mito, Maziwa na Misitu
yote.
Kubadilishana na haki hizo, Mandara alihakikishiwa
ulinzi, yeye na mali zake, pamoja na elimu kwa watoto wake. Akitoa shukrani kwa
Dakta Juhlke na GEAC, Mandara alisema: “Nawapenda sana Wajerumani kuliko
mataifa mengine yote; zaidi kuliko Waingereza hasa, nani kwako pekee (wewe
Juhlke) nitatoa nchi yangu”.
Hatimaye, baada ya kubaini kwamba alikuwa njia
panda, Mandara alilalama akisema: “Sultani wa Zanzibar anataka nchi
yangu; Wajerumani, vivyo hivyo nao wanataka nchi yangu; ninyi (Waingereza)
mnataka nchi yangu pia! Aitakaye nchi yangu atakiona cha mtema kuni”. Hakutaja
aina ya “cha mtema kuni” hicho.
Tume ya maridhiano yaundwa
Kutokana na kindumbwendumbwe hicho, Uingereza,
Ufaransa na Ujerumani ziliunda Tume ya Maridhiano kubainisha mipaka kwa
kuzingatia maeneo ya ushawishi wa nchi hizo kuepuka ugomvi, lakini Sultani
hakushirikishwa.
Mijadala ndani ya Tume ilikuwa mikali, kila
mshiriki akivutia upande wake. Mwakilishi wa Ujerumani alitaka kutumia
Bandari ya Dar es Salaam iliyokuwa chini ya himaya ya Sultani, bila kutozwa
kodi.
Pili, alitaka Sultani apunguziwe eneo la himaya
upande wa Pwani ili abakie na urefu wa maili kumi tu; pia kwamba, madai ya
Sultani huyo juu ya eneo la Kilimanjaro yasitambuliwe.
Tatu, Ujerumani ilitaka kampuni zote za Uingereza
zilizokuwa eneo la Kilimanjaro ziondoke na zikubali kulipwa fidia ili Mjerumani
ashike eneo lote hilo.
Kwa GEAC, Kilimanjaro lilikuwa jambo la kufa na
kupona, na ilikuwa tayari kwa lolote kutoiachia; kama ambavyo tu Zanzibar
ilivyokuwa muhimu kisiasa na kiuchumi kwa “Emperor” Bismarck wa Ujerumani
kiasi kwamba, nchi hiyo ilikuwa na Ubalozi mdogo Visiwani humo tangu mwaka 1884
kuonesha umuhimu huo.
Uingereza na Ufaransa zilionesha kuunga mkono madai
ya Sultani dhidi ya matakwa ya Ujerumani. Kwa kupewa ujasiri na msimamo wa nchi
hizo, wakati mazungumzo yakiendelea, Sultani alituma kikosi chenye Askari 200,
kikiongozwa na Jemedari wa Kiingereza, Jenerali Mathews, kwenda eneo la
Kilimanjaro kusimika bendera nyekundu ya himaya yake. Wakati wakirejea,
walipambana na Kikosi cha Wajerumani karibu na Taveta, kilichofika huko kwa
madhumuni hayo hayo; mapigano yakazuka, lakini yakakoma sawia kwa maelekezo ya
Tume ya Maridhiano iliyokuwa ikiendelea na kikao.
Wakati huo huo, Mwakilishi wa Uingereza, Sir Percy
Anderson, alikuja na wazo la kati katika kutatua ugomvi wa Ujerumani na
Uingereza kuhusu eneo la Kilimanjaro, la kuligawa sehemu mbili kuwapa
Wajerumani nusu ya upande wa Kusini, na nusu ya Kaskazini wapewe Waingereza.
Pendekezo hilo lilipingwa vikali na Wajerumani kwa
madai kwamba isingekuwa rahisi kuligawa hivyo eneo hilo lenye mlima na vilima,
hivyo wakasisitiza wapewe eneo lote peke yao. Sir Percy alitupa hoja yake kutafuta
suluhu mbadala.
Mombasa yatibua mambo
Ikazuka hoja kuhusu nani adhibiti Mombasa (bandari)
ambayo ilikuwa chini ya himaya ya Sultani, lakini yenye kuwaniwa vikali na
Uingereza na Ujerumani pia. Wajerumani walitaka wawe na Bandari Pwani ya
eneo hilo na (iwe) njia fupi kuufikia Mlima Kilimanjaro kwa urahisi, na kwamba,
Mombasa ulikidhi madhumuni haya kwavile ulikuwa katikati ya maeneo ambayo
Ujerumani ilikuwa ikiwania upande wa Kaskazini na Kusini.
Waingereza hawakuwa tayari kupoteza Mombasa, kufa
na kupona; kama ambavyo tu Wajerumani hawakuwa tayari kupoteza Kilimanjaro.
Jemadari wa Kiingereza, Luteni Kanali Kitchner, tayari alikuwa ameshinikiza
kukamatwa kwa Mombasa ili kiwe Kituo cha Manowari zakivita za Uingereza na
ghala kuu la silaha katika bahari ya Hindi.
Nao wafanyabiashara na Wamissionari wa
Kiingereza,walioweka vituo na Makao Mombasa, hawakutaka Serikali yao kuachia
bandari hiyo pamoja na njia za biashara “kuangukia kwenye udhibiti wa Taifa
shindani” kwani, kwa maoni ya Sir Percy, Uingereza ingekosabarabara ya uhakika
hadi Ziwa Victoria “unakoanzia Mto Nile,na hivyo kuwa vigumu kuifikia Sudani ya
Chini”. Kufikia hapo, mazungumzo yaligota na hali ya kutoaminiana kutawala.
Mpaka mpya: Taveta hadi Victoria
Ili kukidhi matarajio yake, Sir Percy aliwasilisha
pendekezo la pili, la Mpaka unaoanzia Kusini mwa Mombasa kuelekea Taveta, kisha
unapanda juu sehemu ya Kaskazini mwa Kilimanjaro (kuuingiza ndani mlima huo),
na kuambaa hadi Mashariki mwa kingo za Ziwa Victoria, kama unavyoonekana leo.
Kwa pendekezo hili la pili, Ujerumani iliamua
kuachia Mombasa na kukubali kutia sahihi Mkataba wa makubaliano kwa kuridhika
kwamba maeneo Kusini ya mpaka huo yaliyobakia mikononi mwake, yalikidhi kiu
yake ya makoloni kufanya ijishughulishe kwa muda mrefu uliofuata.
Mkataba huo, uliofikiwa Novemba 1, 1886, ulielezea
mpaka huo ifuatavyo: “Mstari wa Mpaka unaanzia kwenye mdomo wa Mto Wanga
au Umbe,unakwenda moja kwa moja hadi Ziwa Jipe; unapita upande wa Mashariki mwa
Ziwa na kupinda tena upande wa Kaskazini kabla ya kuvuka mto Rumi; kisha
unachana katikati ya nchi ya Taveita (Taveta) na Uchagga; unaambaa chini ya
kitako cha Mlima Kilimanjaro kwenda juu kuelekea Kaskazini; kisha unanyooka
tena moja kwa moja na kutua upande wa Mashariki wa kingo za Ziwa Victoria
Nyanza”.
Huo ndio ufafanuzi kwa maneno ya kidiplomasia, wa
Mpaka kati ya Tanganyika (wakati huo ikiitwa Deutch – Ostafrika) na Kenya
uliopo hadi leo. Chini ya makubaliano hayo, Ujerumani, kupitia Kampuni ya GEAC,
ilijipatia Mlima Kilimanjaro na kupoteza Mombasa; na Waingereza kujipatia
Mombasa na kupoteza Mlima Kilimanjaro.
Januari 1, 1891, maeneo yote ya GEAC yaliingizwa
kwenye himaya ya Serikali ya Ujerumani kuruhusu uvamizi na uingiliaji kijeshi
wa maeneo hayo,yakiwa tayari milki halali ya nchi hiyo.
Kutoka Deutch – Ostafrika hadi Tanganyika
Sultani wa Zanzibar kwa upande wake, alibakiziwa
kipande cha urefu wa maili 10 tu za Pwani, ambacho miaka miwili baadaye, mwaka
1888, alikikodisha kwa Wajerumani kisha akapokonywa kwa nguvu mwaka huo huo na
Wajerumani hao.
Wakati wa utawala wa Kijerumani, nchi yetu iliitwa
“Deutch – Ostafrika”; na baada ya vita ya kwanza ya Dunia mwaka 1918, ambapo
Waingereza walichukua nchi kutoka kwa Wajerumani, iliitwa “Tanganyika
Territory”, jina lililopendekezwa na Mwingereza, Sir Cosmo Parkinson, kabla ya
kuitwa kwa kifupi “Tanganyika” baada ya vita ya tatu ya Dunia, mwaka 1945.
Mipaka rasmi ya iliyokuwa “Deutch –Ostafrika”
(Tanganyika), iliridhiwa Machi 22, 1921, kufuatia Mkataba wa amani uliofikiwa
kati ya Uingereza na Ujerumani ambapo, kabla ya hapo, eneo lote la sasa la
Kigoma na Biharamulo, lilikuwa chini ya Wabelgiji.
Kwa madhumuni ya mada hiini kwamba, Mlima
Kilimanjaro upo Tanzania kwa sababu mji wa Mombasa uko Kenya, ikiwa ni matokeo
ya minyukano ya mataifa mawili ya Kikoloni, Ujerumani na Uingereza. Na
hilo hatuna nguvu nalo kwa kuwa historia sharti itawale.
Hapa tunapata fundisho pia; kwamba, Watawala wetu
wa leo, wanaoingia Mikataba kimbumbumbu na kizembe na kina “Karl Peters” wa
zama hizi,katika madini na ardhi, kama walivyofanya Chifu Mangungu wa Musovelo
[Usagara] na Chifu Mandara wa Moshi; waelewe kwamba, wanatuweka rehani
kwa wawekezaji hao chini ya ukoloni mpya, sisi na hatima yetu. Kwa sababu
hii, tusishangae kuona siku mojatukivamiwa na wawekezaji hao, wakitumia majeshi
ya nchi mama, pale tutakapoamka kutoka usingizini kudai ardhi rasilimali
tunazoporwa. Huku ni kukaribisha historia kujirudia, kwa kilio na kusaga
meno.
-See more at: http://www.raiamwema.co.tz/kwa-nini-mlima-kilimanjaro-uko-tanzania-na-si-kenya#sthash.6k84Pgqy.dpuf
(Chanzo: Raia Mwema).
No comments:
Post a Comment