Nini kilitokea vifo vya mahabusu Mbeya? IV
Shaban Kaluse
Toleo la 318
2 Oct 2013
Wiki iliyopita tulianza mapitio ya hukumu ya kesi dhidi ya watuhumiwa wa tukio la vifo vya mahabusu mkoani Mbeya. Endelea na sehemu hii ya nne ya mfululizo wa kesi hii.
KATIKA hukumu yake Jaji Lukelelwa alisema; “Kwanza nitaeleza kigezo cha kwanza cha kosa la kuua kwa uzembe, kwamba ni kweli watuhumiwa walikuwa na jukumu la kuwa waangalizi wa mahabusu waliokuwa wamewekwa rumande.
“Kwa mujibu wa kifungu cha 14 cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kama ilivyofanyiwa marekebisho kinasema kwamba, kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka kwa jamii hifadhi ya maisha yake, kwa mujibu wa sheria.
Jaji Lukelelwa aliendelea na hukumu yake akisema; “Watuhumiwa walikuwa na wajibu wa kuhakikisha usalama wa marehemu ambao walikuwa wamewekwa mahabusu. Pia watuhumiwa hawakuwa makini kutekeleza majukumu yao.
Akaendelea; “Sasa nitaelezea sababu ya vifo vya marehemu hao na kama vifo hivyo vimetokana na uzembe wa watuhumiwa. Katika ripoti ya uchunguzi wa miili ya marehemu, ambayo ni kidhibiti cha kwanza (Exhibit No. 1), inaeleza kwamba, marehemu wote 17 walikufa kutokana na kukosa hewa kwa mujibu wa shahidi wa 12 katika kesi hii, Daktari Yunus R. Mbaga, ambaye ni mwanapatholojia anayefanya kazi katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya.”
Katika ripoti yake, Dk. Yunus R. Mbaga, alisema kwamba, ukosefu wa hewa ndio uliosababisha vifo vya mahabusu hao, kama inavyojulikana hewa ya oksijeni ni muhimu katika uhai wa kiumbe chochote.
Hata hivyo, katika ripoti hiyo daktari huyo hakuieleza Mahakama kwa undani ni kiwango gani cha hewa kinahitajika ili mtu aweze kumudu kuishi au mtu anaweza kukaa kwa muda gani bila kupata hewa na akamudu kuishi. Suala hapa ni kujua, ni nani alisababisha mahabusu wale kukosa hewa hadi wakafa.
Lakini katika hukumu yake, pamoja na mambo mengine Jaji aliainisha makosa ya kuua bila kukusudia kama yalivyoelezwa katika ibara ya 195 (1), ya kanuni ya adhabu, inayoelezea kwamba, “mtu yeyote ambaye ametenda kosa kinyume cha sheria na kusababisha kifo cha mtu mwingine, ana hatia ya kuua bila kukusudia.”
Jaji Lukelelwa aliendelea kutoa tafsiri ya sababu za mauaji yanayofanana na kesi husika kwa kunukuu ibara ya 203 (d) na (e) ya kanuni ya adhabu, kisha akaendelea kusema kwamba, mpaka hapo, hakuna mjadala kutokana ushahidi uliotolewa, kwamba, mahabusu waliowekwa rumande katika chumba cha mahabusu kilichopo katika Kituo cha Polisi Rujewa, hakikuwa na uwezo wa kutosheleza idadi ya mahabusu 112 waliowekwa humo.
Akaendelea kusema; “Ili niweze kufikia uamuzi kwamba huenda watuhumiwa walishindwa kutekeleza majukumu yao mpaka wakasababisha madhara ni lazima izingatiwe, ukiachana na majukumu yao ya kulinda usalama na maisha ya mahabusu, watuhumiwa walikuwa pia na majukumu mengine ya kuhakikisha kwamba, wale wafungwa hawatoroki kutoka katika chumba hicho cha mahabusu na walikuwa pia na wajibu mwingine wa kutii amri zote za kisheria ambazo zinatolewa na viongozi wao wa juu wa polisi, ikiwemo sheria na kanuni zinazoendana na Jeshi la Polisi (PGO).
“.....lazima kuwepo mipaka ya uzembe ambayo inaadhibika kama kosa la jinai.
Kwamba uzembe wa washitakiwa ulivuka mipaka na kutothamini maisha na usalama wa wengine hadi kusababisha kosa dhidi ya nchi na linastahili adhabu.
Kesi mbalimbali za kimataifa zilirejewa katika hukumu hiyo ya Jaji Lukelelwa. Kwa mfano, baadhi ya kesi nchini Uingereza katika Visiwa vya Wales ambako kwa miaka mingi mahakama zimekuwa zikitumia maneno, recklessness na gross negligence kuelezea kosa linalosababisha involuntary manslaughter (kuua bila kukusudia) badala ya constructive manslaughter (kuua kwa kukusudia) bila maelezo sahihi ya makosa hayo. Huko, haikuwahi kuwekwa wazi kama maneno hayo yalikuwa ni njia tofauti za kuelezea jambo moja au kueleza hali mbili tofauti zinasababisha kosa kutendwa.
Jaji alioanisha mifano kadhaa ya kesi nchini Uingereza na kesi hiyo ya mahabusu Mbeya na kisha akasema, ushahidi umethibitisha kwamba, kulikuwa na uzembe uliopitiliza ambao ulisababisha kutokea kwa vifo vya mahabusu 17.
Kusafirishwa kwa idadi kubwa ya mahabusu kutoka gereza la Ruanda hadi Rujewa na kuhifadhiwa katika chumba cha mahabusu ya Kituo cha Polisi Rujewa, kitendo ambacho kilifanywa na mamlaka husika ambayo ni Wizara ya Mambo ya Ndani, ni kitendo cha uzembe kwa kiasi fulani.
Kitendo cha Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Rujewa kutokufanya maandalizi stahiki ya kupokea mahabusu hao na kuangalia uwezekano wa kuwahamisha baadhi yao katika baadhi ya vituo vya polisi vilivyokuwa karibu, ni uzembe mwingine.
Kitendo cha Mkuu wa Kituo cha Polisi Rujewa kutokukagua chumba cha mahabusu kutokana na mazingira yaliyojitokeza nao pia ni uzembe. Kitendo cha kutofungua mlango wa ndani wa mbao kutokana na vilio vya mahabusu waliokuwa wamekosa hewa na kujaribu kutafuta sababu za kufanya hivyo, nao pia ni uzembe uliopitiliza au ni kosa la kisheria la uzembe.Chanzo: Raia Mwema.
- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/nini-kilitokea-vifo-vya-mahabusu-mbeya-iv#sthash.cdBQ1gDk.dpuf
No comments:
Post a Comment