CHINA NA DOSARI YA UBORA WA BIDHAA
Njonjo Mfaume
China
Toleo la 318
2 Oct 2013
WIKI hii nilikumbushwa kuwa kasi yangu ya kujifunza kichina ni ndogo sana na nahitajika kujitahidi zaidi baada ya kupata mkasa ambao nusra ungenisababishia kufedheheka vibaya kwenye jumuia.
Mapema siku ya tukio nilihudhuria darasani na kisha baada ya kutoka nikaenda kula, ambapo nilijaribu mlo mpya wa wali na mayai ya kukaanga yaliyochanganywa na nyanya mbichi.
Baada ya mlo, nikaanza safari kuelekea Ofisi ya Afya hapa Shanghai kwa ajili ya vipimo, ikiwa ni sehemu ya mchakato wa kupata kibali cha kuishi China.
Nikiwa njiani kwenye treni, tumbo likaanza ‘kero’: maumivu kidogo, mara ‘grrr’, mara linanyonga. Niliendelea na safari nikiamini ni mtibuko mdogo wa tumbo ambao hautadumu.
Kituo kimoja kimoja kabla ya kushuka, tumbo likichachamaa hadi hamu ya safari ilinitoka na kuanza kusali nikiomba Mungu anihifadhi. Juhudi za kutafuta maliwato niliposhuka kituoni zilipogonga mwamba, nikalazimika kuuliza ingawa wakati huo, maumivu ya tumbo yalinivuruga kiasi cha kusahau sentensi na maneno machache za Kichina niliyojifunza.
Kila abiria niliyemuuliza, aidha hakujua kiingereza au kichina nilichotumia hakikunyooka na hivyo ikawa kama napigia mbuzi gitaa.
Muongoza treni akiwa na kibendera-ishara chake ndie aliyeokoa jahazi. Alijua naumwa na nahitaji msaada wa haraka. Alisimama na kupiga ukelele uliosikika kituo kizima akirudia mara kadhaa …ingliiiish.. ingliiish, mwito ambao ulimleta abiria mmoja aliyejua kiingereza na kusaidia kuniulizia.
Unaweza kunilaumu kwa kushindwa kuwasiliana kichina hata baada ya kuhudhuria madarasa ya lugha hiyo kwa takriban wiki mbili; lakini ukweli ni kwamba Kichina ni kigumu.
Ugumu wake upo katika matamshi. Hii ni lugha ya toni (tone) ambapo maana ya neno inategemea na jinsi unavyolitamka. Nieleweke, sio baadhi ya maneno, bali maneno yote yatakuwa na maana uliyoikusudia tu kama ulitamka kwa toni sahihi. Kila neno la mandarin lina toni yake.
Toni, walimu wanasisitiza ndio kila kitu. Neno ‘ma’, kwa kadiri ya unavyolitamka linaweza kumaanisha mama, malighafi ya kutengenezea nguo, punda, kulaani au kukaripia, safisha au linaweza kuwa ni kiulizo.
Katika kuonesha umuhimu wa toni, somo la kwanza kufunzwa lilikuwa ni toni tano za mandarin na mpaka sasa kila mwalimu anayekuja darasani anaanza na mazoezi ya toni kabla ya kuendelea na somo la siku hiyo.
Katika safari yangu ile iliyoniletea zahama ya tumbo, wakati wa vipimo katika kituo kile cha afya watu hutakiwa kuvua nguo zao na kuvaa nguo za maabara ambapo ukivua nguo, unaweka katika droo ndogo na kuchukua ufunguo.
Mmoja kati ya walioenda kupima alichanganya namba na kuweka vitu vyake katika droo isiyo yake. Aligundua hilo baadaye wakati anataka kuchukua vitu vyake. Alipofungua droo la namba ya ufunguo hakukuwa na kitu. Alipofikiria zaidi, akagundua droo aliloweka vitu vyake ni pembeni ya lile. Lakini ufunguo ule ulifungua na kufunga kitasa cha droo isiyo ya namba yake, alimoweka vitu vyake.
Ubora wa bidhaa ni jambo muhimu hata kama ni kwa kitu kidogo kama ufunguo wa kitasa. Vitasa vile vya droo ni miongoni mwa bidhaa maarufu za China, nchi ambayo ubora wa bidhaa ni suala tete ambalo linatishia sifa zake nyingine nzuri.
Wiki iliyopita nilitaja kuwa Wachina ni wachapakazi na hata watu wa mataifa ya magharibi na dunia nzima wanakiri hilo. Hata hivyo, moja kati ya ukosoaji mkubwa dhidi ya China ni uduni wa bidhaa zao.
Ila kwamba China ni mzalishaji wa bidhaa duni imeenea dunia nzima. Nchi zote zinazofanya biashara na Wachina zimewahi kulalamikia ubora wa bidhaa. Kadhalika, hata Wachina wenyewe wana hofu ya ubora wa bidhaa zao.
Huko nyuma mwaka 2008 kumewahi kuwa na kashfa ya maziwa ya watoto yaliyochakachuliwa na kusababisha watoto zaidi ya 10,000 kuumwa na wachache kufariki. Serikali ya China ilikamata watengenezaji wengi wa bidhaa hiyo na kunyonga wawilli. Tangu wakati huo, wananchi wengi hawaamini maziwa ya watoto yanayotengenezwa nchini mwao, ingawa kama ilivyothibitika vyombo vya habari vya magharibi vinalaumu Serikali ya China kwa kutoshuighulikia tatizo hili. Wanasema Chama cha Kikomunisti cha China kinasaidia kukuza viwanda vya China ambavyo vinaingiza fedha za kigeni lakini hakishughuliki kudhibiti wale wanaokiuka maadili katika biashara.
Kwa upande wa pili, watetezi wa China wanasema watu wanaamini bidhaa za China ni duni kwa sababu ya wingi wa bidhaa zenyewe zinazozalishwa. Wanasema hata asilimia moja ya bidhaa zikiwa duni ni nyingi mno.
Hata hivyo, mwaka 2007 katika uchunguzi uliofanywa na Serikali asilimia 20 ya bidhaa zinazotengenezwa nchini China ziligundulika kuwa ni duni, ingawa uchunguzi huo haukujumuisha bidhaa zilizouzwa nje.
Wachina ni wezi wa teknolojia kiasi kwamba wanakuwa na bidhaa feki ya kila bidhaa asili, na serikali ya China haionyeshi kukwazika na hilo, ukizingatia kuwa nyingi ya bidhaa hizo zinasafirishwa nje.
Hata hivyo, sio kweli kwamba kila bidhaa ya China ni duni. Kuna bidhaa nzuri na za ubora unaotakiwa, lakini ni chache na ngumu kuzipata. Siri kubwa ya kupata bidhaa nzuri ni kununua kwa wakala wa kampuni inayotengeneza bidhaa unayoitaka, baada ya utafiti wako.
Simu za kichina Nilipotaka kununua simu hapa China, mwenyeji wangu alinionyesha tovuti mbalimbali za maduka makubwa na kunielekeza nani anauza bidhaa halisi na nani anauza bidhaa za kughushi. Ingawa maduka yenye shaka bidhaa duni bei ni chee. Mwisho wa siku ni chaguo lako.
Miongoni mwa waathirika wakubwa wa bidhaa feki za China ni nchi zetu masikini kama Tanzania, na hii ni kwa sababu wafanyabiashara hawahangaiki kutafuta bidhaa za ubora unaotakiwa ambazo zipo lakini ni vigumu kuzipata.
Kadhalika, wafanyabiashara wenyewe wa nchi zetu wanataka vitu vya bei rahisi ambayo sio tu vitaendana na uwezo wa wateja wao bali pia vitaweza kuwapatia faida kubwa.
Katika makala moja iliyochapwa katika blog ya mambo ya ushauri wa kisheria inayomilikiwa na Harris Moure ushauri unatolewa jinsi wafanyabiashara wanavyoweza kujihakikishia ubora wa bidhaa wanapofanya biashara na kampuni za China.
Moure anashauri mikataba mizuri ambayo inatambulika katika mfumo wa sheria wa China, anashauri mkataba umpe mnunuzi uwezo wa kuchunguza ubora mara kwa mara na kama kuna tatizo kampuni ya China inayouza bidhaa iwajibike. Kadhalika Moure anashauri kampuni inayonunua bidhaa ifuatilie ubora kwa karibu kwani mkataba pekee bila utekelezaji hautoshi.
Hata hivyo, kwa nchi zetu za Afrika ambazo wafanyabishara ni sehemu ya tatizo na wengi hufika China kuokoteza bidhaa huku na kule, ushauri huu unaweza usiwe na manufaa sana.
Na hapa ndio umuhimu wa kuwa na udhibiti wa bidhaa unaonekana ili kulinda watumiaji. Serikali inayojali watu wake, lazima ihakikishe inawalinda kwa kuhakikisha bidhaa wanazouziwa ni za ubora unaotakiwa.
Tabia ya mwanadamu hasa sisi tunaoishi katika nchi masikini ni kutojali madhara ya muda mrefu yanayotokana na matumizi ya bidhaa duni, lakini tunapoumwa maradhi ya ajabu tunaitegemea Serikali ituhudumie.
Mwaka jana iliripotiwa kuwa Serikali ya China iliahidi kuzuia usafirishwaji wa bidhaa duni kwenda nchi za Afrika. Je, bidhaa feki kutoka China zimekoma? Nina wasiwasi na hilo.
Jambo la kuvutia ni kwamba katika chanzo hicho hicho nilichosoma kuhusu ahadi hiyo, maofisa wa China pia walilaumu wafanyabiashara wa Afrika na kuzitaka nchi za Afrika kutunga sheria kali. Tunarudi pale pale Serikali, Serikali, Serikali. Chanzo: Raia Mwema.
- Angalia zaidi at: http://www.raiamwema.co.tz/china-na-dosari-ya-uduni-wa-bidhaa#sthash.a5eKbToe.dpuf
No comments:
Post a Comment